JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UPOTOSHWAJI WA UGONJWA WA HOMA YA DENGUE
Wizara
ya Afya na Ustawi wa jamii inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa
mbalimbali za upotoshaji unaofanywa kupitia baadhi ya mitandao ya
kijamii, simu za mikononi na mikusanyiko ya watu kuwa ugonjwa wa Dengue
haupo nchini Tanzania.
Wizara inapenda kusisitiza kwamba, ugonjwa huo upo nchini na serikali
kwa kushirikiana na wananchi inaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za
kukabiliana nao. Ikumbukwe ugonjwa huu unapatikana pia katika nchi
nyingi duniani zilizoko katika ukanda wa joto na unaathiri takribani
asilimia 40 ya watu duniani.Takwimu za Shirika la Afya Duniani
zinathibitisha kuwa takribani watu milioni 5 wanaripotiwa kuugua ugonjwa
wa kila mwaka.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya Dengue
- Kuangamiza mazalio ya mbu
- Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo
- Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile: vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
- Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
- Hakikisha maua yanayo pandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
- Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara
- Safisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama
- Kujikinga na kuumwa na mbu
- Tumia viuatilifu vya kufukuza mbu “mosquito repellants”
- Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
- Tumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala majira ya mchana na hasa kwa watoto)
- Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Wizara inawakumbusha
wananchi wa Tanzania kuwa, huu ni muda muafaka wa kuzingatia utunzaji
bora wa mazingira yetu. Tukitunza mazingira yetu, nayo yatatutunza na
kutuepusha na maradhi yanayoambatana na mazingira machafu.
Nsachris Mwamwaja
Msemaji wa wizara
23 mei 2014
Msemaji wa wizara
23 mei 2014
No comments:
Post a Comment