Rais wa Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter amefurahishwa na
mipango ya maendeleo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na
kuahidi kusaidia miradi mbalimbali.
Blatter alisema hayo jana
(Mei 22 mwaka huu) ofisini kwake jijini Zurich, Uswisi baada ya kufanya
mazungumzo na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
FIFA itaisaidia
Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo kama Goal, lakini pia
itasaidia kutoa mafunzo kwa makocha, waamuzi wa mpira wa miguu,
madaktari wa tiba ya michezo na watawala.
Vilevile shirikisho
hilo la kimataifa lililoanzishwa mwaka 1904 litasaidia katika ujenzi na
uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya mpira wa miguu nchini Tanzania.
DIT, CBE KUCHEZA FAINALI BEACH SOCCER
Fainali
ya michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (beach soccer) kati ya
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Elimu ya Biashara
(CBE) inachezwa kesho (Mei 25 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One
uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Timu hizo zimepata nafasi
ya kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali dhidi
Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA)
zilizochezwa wikiendi iliyopita.
Mgeni rasmi katika fainali hiyo
anatarajiwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Jamal Malinzi na itaanza saa 4 kamili asubuhi. Fainali hiyo itatanguliwa
na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya AU na TIA kuanzia saa 3
kamili asubuhi.
Michuano hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika
nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar es Salaam, na ilianza Aprili 20
mwaka huu katika fukwe za Escape One na Gorilla iliyopo Kigamboni.
Vyuo
vingine vilivyoshiriki ni Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT),
Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Taasisi ya Ustawi wa
Jamii (ISW) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine ni
Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),
Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na
Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ).
Tanzania itashiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli.
NGORONGORO HEROES YAIVAA NIGERIA
Kikosi
cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heroes) kinashuka uwanja nchini Nigeria kuivaa Nigeria (Flying Eagles)
katika mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika.
Mechi hiyo
itachezwa Leo (Mei 24 mwaka huu) katika Uwanja wa Ahmadou Bello uliopo
katika Jimbo la Kaduna kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa za Nigeria.
Ngorongoro Heroes ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es
Salaam kwa mabao 2-0.
Mwamuzi Alhadi Allaou Mahamat wa Tchad
ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Atasaidiwa na Issa Yaya, Alfred
Madjihoudel na Idriss Biani wote kutoka Tchad. Kamishna ni Aboubakar
Alim Konate wa Cameroon.