expr:class='"loading" + data:blog.mobileClass'>

Friday, March 7, 2014

IJUE SIKU YA WANAWAKE DUNIANI NA TANZANIA







Vuguvugu la Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kupitia kwa wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani walioandamana kupinga mazingira duni ya kazi zao, walilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira. Kutokana na hali hiyo, nchi ya Marekani ilikubali kuwa na siku ya maadhimisho ya kitaifa ili kutafakari masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wa  wanawake.

Hatimaye Umoja wa Mataifa ulipaoanzishwa mwaka 1945; tarehe 8 Machi iliridhiwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa ulitokana na kukubali kwake kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo maalumu na wa pekee.
madhumuni ya maadhimisho

Madhumuni ya kuadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni kuwezesha jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa/ kikanda  na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na wanawake katika kuhakikisha haki za wanawake kiuchumi, kijamii, na kisiasa zinapatikana na zinalidwa.

Aidha, madhumuni mahususi ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo, kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau wengine katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo yao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
utaratibu wa maadhimisho

Tanzania ilianza kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka 1996, maadhimisho yamekuwa yakiandaliwa Kitaifa na katika ngazi ya mkoa. Aidha, nikumbushe kwamba katika maadhimisho ya mwaka 2005 Serikali iliweka utaratibu wa kuandaa Maadhimisho ya Kitaifa kila baada ya miaka minne; ili kutoa fursa maalum kwa mikoa, wilaya na wadau wengine kupima mafanikio yaliyofikiwa katika kumwendeleza mwanamke katika ngazi hizo kwa miaka hiyo na ifikapo mwaka wa tano maadhimisho yafanyike kitaifa kwa kutoa taarifa ya utekelezaji kwa nchi nzima.

Hivyo maadhimisho ya mwaka huu 2014 yanafanyika katika ngazi ya mkoa, na kila Mkoa umeandaa utaratibu wa maadhimisho haya kwa kusisitiza Kaulimbiu ya kimataifa ambayo ni; “CHOCHEA MABADILIKO KULETA USAWA WA KIJINSIA”.

No comments:

Post a Comment